22 Septemba 2022 - 16:37
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu asisitiza kuendelea njia ya mapambano dhidi ya maadui

Akizungumza hivi karibuni katika shehere ya kuwaenzi maveterani wa vita vya kujitetea kutakatifu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba ilithibitika wazi katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu kwamba ulinzi wa nchi na kuzuia vitisho vya adui hakutimii kwa kusalimu amri, bali kwa kusimama imara na kudumisha mapambano.

Ikiwa ni katika mkesha wa maadhimisho ya Wiki ya Kujitetea Kutakatifu, maveterani wa vita, makamanda na wapiganaji wa vita vya kujitetea kutakatifu na familia za mashahidi walikutana siku ya Jumatano asubuhi na Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ukumbi wa Husseiniyah ya Imam Khomeini (MA).

Katika maadhimisho hayo, Ayatullah Khamene alisema kwamba vita hivyo vilisababishwa na sera za kistratijia za mabeberu za kuchochea uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran na kuongeza: Licha ya ungaji mkono mkubwa na wa pande zote wa mataifa yenye nguvu duniani kwa Saddam mwenye tamaa na uchu wa madaraka, lakini vita hivyo viligeuka kutoka kuwa tishio la uhakika na kubwa na kuwa fursa kubwa kwa msingi wa vipengele vitatu vya "nguvu ya kihamasa ya mapinduzi, uongozi athirifu wa Imam na sifa za kipekee za taifa shupavu la Iran". Ufafanuzi sahihi na wa kina wa kipindi hicho cha hamasa na cha kusisimua cha historia ya Iran bila shaka utakidhaminia kizazi kipya cha vijana wetu kudumishwa mafanikio ya mapinduzi.

Kwa hakika, vita ambavyo vilianzishwa na madola yenye kiburi duniani kupitia utawala wa Saddam dhidi ya mfumo mchanga wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tarehe 22 Septemba 1980 vilikuwa na malengo kadhaa, ambayo yalikuwa ni ndoto ya kuangushwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, kugawanywa  Iran na kuzuia usambaaji wa ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu katika nchi zilizokuwa chini ya udhibiti wa madola ya kibeberu. Mapinduzi ya taifa la Iran hayakuwa tu kushindwa kwa mfumo tegemezi na mbovu na pigo la muda tu kwa Marekani na madola mengine yenye kiburi, bali yalikuwa tishio kwa utawala wa mfumo mzima wa ubeberu duniani na kwa msingi huo madola yenye kiburi ya Magharibi na Mashariki, yakiwa yanalielewa vyema hilo, yaliamua kulitwisha taifa la Iran vita hivyo kupitia dikteta Saddam.

Ikiwa ndio kwanza ilikuwa imepeta ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu, Iran haikuwa tayari kuingia kwenye vita hivyo haribifu na hatari kwa usalama wake. Zana za kivita na vikosi vya jeshi la Iran vilihitajia ukarabati mkubwa, na maadui, ambao waliona masilahi yao yakiwa hatarini, walikuwa wakitafuta kila fursa ya kuchochea machafuko nchini. Baada ya maadui kushindwa kufikia malengo yao kwa njia hiyo, waliamua kuanzisha vita vya miaka 8 dhidi ya Iran kupitia utawala wa Baath wa Iraq ambao waliendelea kuunga mkono kwa silaha, kifedha na kisiasa katika kipindi chote cha vita vya kulazimishwa dhid ya taifa la Iran.

Mfano wa wazi wa uungaji mkono huo usio na kifani wa madola ya Mashariki na Magharibi kwa Saddam ulionekana wazi pale Marekani na Umoja wa Kisovieti ambazo wakati huo zilikuwa katika Vita Baridi baada ya Vita ViKuu vya Pili vya Dunia, lakini pamoja na hayo ziliamua kuweka kando tofauti na uhasama wao huo na kumpa Saddam kila aina ya msaada aliohitaji wa silaha, fedha na siasa kwa ajili ya kupambana na Iran.

Pamoja na hayo, lakini wananchi wa Iran ya Kiislamu, chini ya uongozi wa Imam Khomeini (MA) na kwa mapambano ya dhati, sio tu waliwashinda maadui zao, bali pia waliacha mafanikio ya kipekee katika mfumo wa utamaduni wa mapambano, mafanikio ambayo ni mfano wa kudumu kwa taifa la Iran na Ummah mzima wa Uislamu katika uwanja wa kutetea thamani za kimaadili na kukabiliana na vitisho vya maadui.

Mafanikio mengine ya kujitetea kutakatifu ni kusimamishwa dola la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa kimataifa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kufuatia kujitetea huko kutakatifu, maadui walitambua kwamba mfumo wa Kiislamu wa Iran hauwezi kupinduliwa kupitia mashambulizi ya kijeshi.

Kuzuia hujuma ya adui, kujitosheleza katika nyanja tofauti na mkakati wa kutegemea zana za kivita zinazotengenezwa ndani ya nchi katika sekta ya ulinzi ni miongoni mwa mafanikio mengine ya kujitetea huko kutakatifu. Kutokana na maendeleo makubwa iliyoyapata Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uwanja wa kutengeneza silaha tofauti, yakiwemo makombora na droni, hivi sasa Iran iko katika kiwango cha juu cha kuzuia hujuma ya maadui ambapo mbali na kujidhaminia mahitaji yake ya ndani, ni miongoni mwa nchi zinazouza nje silaha na zana za kijeshi.

Kuhusu suala hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasisitiza kwamba: "Kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, hii leo nchi imefikia hatua ya kuzuia mashambulizi ya adui na wala hakuna wasiwasi wowote kuhusu vitisho vya nje, na maadui pia wanalijua vizuri suala hili."

/